Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii imeadhimisha siku ya Mtoto wa Afrika katika shule ya msingi Chalinze ikiwa na kauli mbiu isemayo “Tuimarishe ulinzi wa mtoto,tokomeza ukatili dhidi yake: jiandae kuhesabiwa” ambapo kauli mbiu hiyo inaikumbusha jamii juu ya kulinda haki za watoto ilikupata jamii bora inayojali usawa na pia kusisitiza watu wote kuhesabiwa katika zoezi la sensa ya watu na makazi itakayofanyika tarehe 23 Agosti,2022 siku ya jumanne.
Katika hafla hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Chalinze Ndg.Ramadhan Possi ambaye ndiye mgeni rasmi amekabidhi vifaa nbalimbali kwa watoto wenye mahitaji maalum katika shule mbili za Msingi ambazo ni shule ya msingi Chalinze pamoja na shule ya msingi Msoga ikiwa ni ishara ya kuiunga mkono Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Maendeleo ya jamii katika sera yake ya kutambua umuhimu wa mtoto nchini.
Aidha Ndugu Mgeni rasmi ametoa hotuba fupi ikiwa ni mara baada ya kusomwa kwa risala kutoka kwa wananfunzi wa Shule ya msingi Chalinze ambapo amesema serikali imeendelea kuhakikisha mtoto anapata haki yake ya Msingi ya kuishi na imechukua hatua kadhaa dhidi ya kuwakinga watoto ikiwa ni pamoja na kampeni za chanjo.
“Katika kuhakikisha kwamba mtoto anapata haki yake ya msingi ya kuishi, Serikali imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha usalama wa mama na mtoto kabla ya kujjifungua na hivyo huduma za mamam wajawazito na watoto walio chini ya miaka mitano hutolewa bure katika zahanati na vituo vya Afya. Na vilevile Serikali imechukua hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na kampeni za chanjo ya kuzuia ulemavu utotoni kama vile polio, kutunga sharia zinazolinda maslahi na kuboresha maisha ya watoto”. Amesema Ndg. Ramadhani Possi.
Aidha Ndg.Ramadhani Possi amesema kuwa ili kuendana na kauli mbiu ya siku ya mtoto wa Afrika kwa mwaka huu 2022 Serikali na jamii haina budi kufanya mambo mbalimbali ikiwemo kuhamasisha na kuelimisha jamii juu ya haki za watoto ili kuondoa dhana potofu,kuhamasisha jami kuhusuwatoto kupata chanjo,kamati za shule ziwemstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa ujenzi wamajengo ya shule unazingatia hali za walemavu na pia kutambua matatizo,kupanga,kutekeleza,kusimamia na kutathimini miradi mbalimbali itayosaidia watoto walemavu na watoto wengine.
Nae Mkuu wa idara ya Maendeleo ya jamii Bi Nyamayao Said amelishukuru Shirika la PASADA kwa kushirikiana na Halmashauri ya Chalinze kwa kuwathamini watoto katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika ambapo vifaa mbalimbali vimegawiwa kwa wanafunzi wenye uhitaji amabvyo vimegharimu jumla ya Tsh1,608,00/=.
“Niwashukuru Shirika la PASADA kwa ,kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze kwa kuweza kuwafikia watoto hawa katika siku hii muhimu ya Siku ya Mtoto wa Afrika ambapo Halmashauri ya Chalinze imekabidhi vifaa kama vile sabuni,mafuta ya kupaka ,miswaki,sukari,pampasi na viburudisho vyenye thamani ya Tsh.1,208,000/= na Tsh 400,000/= kutoka Shirika la PASADA kwa jumla ya watoto 40 wenye mahitaji na changamoto ambapo watoto 20 wametoka katika shule ya Msingi Chalinze na watoto 20 kutoka shule ya msingi Msoga”. Amesema Bi.Nyamayao.
Kwa upande wa Diwani wa kata ya Pera Mhe. Jackson Mkango ameipongeza Serikali na Halmashauri ya Chalinze kwa ujumla kwa kuhakikisha inaweka mazingira mazuri ya haki na ustawi wa watoto.
Kwaniaba ya Wananchi wa Pera tumefurahi kwa maadhimisho haya kufanyika hapa na tunaishukuru Serikali na Halmashauri yetu ya Chalinze kwa kuhakikisha inaweka mazingira mazuri ya usalama, haki na ustawi kwa mtoto na kuthibitisha hilo tutamalizia ujenzi wa bweni la watoto wenye mahitaji maalumu kuanzia wiki ijayo2”.Amesema Mhe. Mkango.
Aidha Mhe. Mkango amewaomba wadau mbalimbali kushirikiana na Halmashauri ya Chalinze kuendelea kujitoa na kuunga mkono jitihada za Serikali katika kujenga na kuimarisha haki na ustawi wa watoto wetu.
Ikumbukwe kuwa Kila ifikapo Tarehe 16,juni kila Mwaka huwa ni siku ya Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika ambapo maadhimisho haya yalianza kuadhimishwa mnamo mwaka 1991 ikiwa ni maadhimio ya kukumbuka uasi dhidi ya wanafunzi uliotokea mnamo tarehe 16,juni,1976 huko Soweto,Afrika Kusini ikiwa na lengo la kuwakumbusha watoto hatua ya kijasiri waliyoichukua wenzao huko Afrika Kusini katika kulinda utu,heshima na haki zao za msingi.
114 Morogoro Rd, 61383 Bwilingu
Anuani ya posta: P O BOX 65 Chalinze
Simu: +255232935403
Simu ya mkononi:
Barua pepe : ded@chalinzedc.go.tz
Copyright ©2018 chalinze district council . All rights reserved.