Shirika lisilo la kiserikali la Doris Mollel Foundation hii leo limekabidhi vifaa tiba vyenye thamani ya Tsh Mil.12 katika Hospitali ya Wilaya iliyopo Msoga ambapo vifaa hivyo vilivyokabidhiwa mbele ya Naibu Waziri wa Ardhi ,nyumba na maendeleo ya makazi na pia Mbunge wa Jimbo la Chalinze na Mhe. Ridhiwani Kikwete ni pamoja na Mashine tatu za kutolea au kufua hewa ya Oxygen.
Akizungumza mara baada ya makabidhiano hayo Mkurugenzi wa taasisi hiyo Bi.Doris Mollel ametoa pongezi kwa Mhe Rais wa Tanzania kwa kuweka mazingira bora ya taasisi hizo zisizo za Kiserikali kufanya kazi kwa ufanisi.
“Tunaishukuru sana Serikali na Rais wetu Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira bora kwa sisi mashirika yasio ya kiserikali ili tuweze kufanya vizuri na ndio maana tunashirikiana na Shirika la Kimarekani la Segal Family Foundation kutoa vifaa hivi na ndio maana hii leo tumeleta Mashine 3 za kutolea hewa ya Oksijeni (Oxygen) kwa watoto wanaozaliwa kabla ya wakati yaani njiti zikiwa na uwezo wa kuhudumia watoto wawili kwa kila mashine kwa wakati mmoja”. Amesema Bi Doris
Hata hivyo ameendelea kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Chalinze kwa jitihada za kutafuta na kuwakumbusha shirika lao kufika katika Hospitali ya Wilaya kuweza kuwahudumia wana Chalinze.
Aidha Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya Dkt. Allen Mlekwa amelishukuru Shirika la Doris Mollel Foundation kwa msaada walioipatia hospitali hiyo kwani vitasaidia upatikanaji wa huduma bora kwa watoto njiti.
“Kikubwa tunakushukuru kwa vifaa hivi kwani vimekuja wakati muafaka kwasababu tumeanzisha huduma na jengo la mama na mtoto hivyo basi tumepata vifaa kutoka Serikali kuu lakini pia kwa msaada wa Mashine hizi imetusaidia kuweza kuwahudumia watoto watakaozaliwa kabla ya wakati.” Amesema Dkt. Mlekwa.
Aidha Naibu Waziri wa Ardhi ,nyumba na maendeleo ya makazi Mhe. Ridhiwani Kikwete(mb) ametoa neno la shukrani kwaniaba ya wananchi wa Chalinze kwa Shirika hilo kwa msaada wa vifaa tiba kwani vitasaidia kuhudumia kundi la watoto watakaozaliwa kabla ya muda wao.
“Kwaniaba ya wanachalinze nikushukuru sana Mkurugenzi na taasisi yako kwa kujitolea na kwa msaada huu kwani Tanzania ni kubwa na ina maeneo mengi lakini ukaona kwa ulicho nacho uanze na Chalinze na msaada huu una maana kubwa sana hasa kwenye kundi linalokwenda kusaidiwa ambao ni watoto njiti kwanii kundi hili kwa Chalinze linatupa changamoto kwenye kuwalea mpaka kufikia wao kujitegemea hivyo basi kupitia msaada huu na misaada mingine uliotuahidi umetusadia kuimarisha na kuokoa afya na uhai wa watoto hao”. Amesema. Mhe Ridhiwani.
Aidha Mhe. Ridhiwani amemuahidi Mkurugenzi wa Doris Mollel Foundation kuwa atazifikisha salamu kwa Mheshimiwa Rais ili afahamu ni kwa jinsi gani ameamua kuwasaidia wana Chalinze na wananchi kwa ujumla kupitia taasisi yake.
114 Morogoro Rd, 61383 Bwilingu
Anuani ya posta: P O BOX 65 Chalinze
Simu: +255232935403
Simu ya mkononi:
Barua pepe : ded@chalinzedc.go.tz
Copyright ©2018 chalinze district council . All rights reserved.