Wenyeviti wa kamati za Kudumu za Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze wakiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chalinze wametembelea leo viwanja vya nanenane katika Manispaa ya Morogoro na kufika katika Banda la maonesho la Halmashauri ya Chalinze na kujionea shughuli mbalimbali za uzalishaji kama kilimo cha mbogamboga,ufugaji wa Mifugo mbalimbali kama kuku,ng’ombe na mbuzi,pia wameweza kukakagua shughuli mbalimbali za wajasiriamali wanawake na vijana wanaokopeshwa na Halmashauri ya Chalinze.
Katika ziara hiyo wenyeviti wa kamati za Kudumu waliweza kujionea shughuli za wajasiriamali wanaozalisha sabuni,mafuta ya ngozi,ungalishe,unga wa mahindi wa sembe na dona,watengeneza vinyago na watengeneza batiki na mapambo mbalimbali ya nyumbani.
Mwenyekiti wa Halmashauri Mheshimiwa Hassani Mwinyikondo alifurahishwa na shughuli zinazotekelezwa na Halmashauri ya Chalinze hususan katika sekta ya kilimo na mifugo na kuwataka wataalam katika sekta hizo kuyatekeleza mazuri hayo katika vijiji wanakofanyia kazi .”Niwaombe wataalam wangu matendo haya ya kilimo cha kisasa na ufugaji wa kisasa mkayafanyie kazi kwa kuwaelimisha wananchi kwa vitendo ili tukawe na Kilimo chenye tija yasiishie kwenye maonesho tu.” Mwinyikondo ameyasema hayo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya Uchumi,Ujenzi na Mazingira,Mheshimiwa Malota Kwaga aliwapongeza wajasiriamali wa Halmashauri ya Chalinze kwa jinsi wanavyoitendea haki mikopo inayotolewa na Halmashauri ya Chalinze kwa kuanzisha miradi endelevu na ya kimkakati inayoweza kuwakwamua kutoka hatua moja kwenda nyingine na hatimaye kuweza kuwa na mitaji imara. “ Nawapongeza sana vijana na wanawake mlivyoweza kubuni na kuanzisha miradi bora na endelevu kutokana na asilimia kumi ya mapato ya ndani hakika mtakuwa mabalozi wema kwa kueleza faida za mikopo inayotolewa na Halmashauri kwa vitendo.” Malota alisema.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri Mheshimiwa Ismail Msumi aliupongeza uongozi wa Halmashauri ya Chalinze na kupongeza juhudi zinazofanywa na wataalam katika kuelimisha wananchi katika maonesho ya nanenane ili sekta ya Kilimo iweze kuchangia pato la taifa asilimia kumi ifikapo mwaka 2030.” Wataalam mkiyafanya maonesho haya kwa vitendo mahali penu pa kazi ajenda ya 10/30 inawezekana.” Msumi alisema
wajasiriamali wakiwa na bidhaa zao katika maonesho ya Nanenane Banda la Chalinze
114 Morogoro Rd, 61383 Bwilingu
Anuani ya posta: P O BOX 65 Chalinze
Simu: +255232935403
Simu ya mkononi:
Barua pepe : ded@chalinzedc.go.tz
Copyright ©2018 chalinze district council . All rights reserved.